Je, Unatafuta Kazi au Ajira?
<< BOFYA HAPA>> Kupata Ajira Yako Leo

Sunday, October 13, 2019

Serikali Kuzipatia Ruzuku Kaya Zote Maskini Nchini Baada Ya Kuridhishwa Na Maendeleo Wanufaika Wa Tasaf

adv1
Na James K. Mwanamyoto-Nyasa
Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) imeahidi kuzinufaisha kaya zote maskini nchini baada ya kuridhishwa na namna wananchi katika vijiji vilivyonufaika na Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini walivyoboresha maisha yao na kujikwamua katika lindi la umaskini liliokuwa likiwakabili.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George H. Mkuchika (Mb) wakati akizungumza na wanufaika na wananchi wa kijiji cha Nangombo wilayani Nyasa akiwa katika ziara yake ya kikazi yenye lengo la kukagua utekelezaji wa Mpango huo wilayani humo.

Mhe. Mkuchika amefafanua kuwa, iwapo wanufaika wasingetumia ruzuku vizuri kuboresha maisha, Serikali isingesita kusimamisha utekelezaji wa Mpango huu wa Kunusuru Kaya Maskini nchini.

“Hongereni wanufaika wa TASAF kijiji cha Nangombo na maeneo mengine kwa kutumia ruzuku kuboresha maisha yenu, kujenga nyumba bora, kununua vifaa vya shule kwa ajili ya watoto na kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi,” Mhe. Mkuchika amepongeza.

Mhe. Mkuchika ameongeza kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano imeridhika na mafanikio yaliyopatikana, hivyo itaendeleza vita dhidi ya umaskini, lengo likiwa ni kuboresha maisha ya kaya zote maskini nchini.

Akiwasilisha taarifa ya kijiji cha Nangombo kuhusu utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini, Afisa Mtendaji wa kijiji hicho, Bw. Joseph P. Ngogi amesema watoto 66 wa shule wananufaika na ruzuku inayotolewa hivyo imeongeza mahudhurio shuleni na kliniki kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano, aidha kaya 65 zimeboresha makazi yao kwa kujenga ama kukarabati na kuezeka kwa bati.

Mmoja wa wanufaika wa Mpango wa TASAF kijiji cha Nangombo, Bi. Mariana Mkwaila amesema ruzuku anayoipata imemuwezesha kuwanunulia watoto wake sare za shule, viatu na madaftari ikiwa ni pamoja na kujenga nyumba kubwa ambayo anatarajia kuizeka kwa bati hivi karibuni.

Naye, Bi. Elizabeth Damian amesema, alikuwa akiishi maisha ya kimaskini kwenye nyumba ya nyasi kabla ya kuingizwa kwenye Mpango, lakini baada ya kuanza kupokea ruzuku ameweza kufuga kuku, mbuzi na kufyatua tofali zilizomuwezesha kujenga nyumba iliyoezekwa kwa bati.

Mhe. Mkuchika amehitimisha ziara yake ya kikazi mkoani Ruvuma kwa kuitembelea Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma na kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wilayani humo.
adv
Loading...

Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
Mgid
taboola apo chini
hapa
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )