Je, Unatafuta Kazi au Ajira?
<< BOFYA HAPA>> Kupata Ajira Yako Leo

Sunday, February 24, 2019

Waziri Mkuu: Tutatekeleza Ahadi Zote Zilizotolewa na Rais Magufuli

juu
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewahakikishia wananchi kwamba ahadi zote zilizotolewa na Rais Dkt. John Magufuli katika maeneo mbalimbali nchini zitakuwa zimetekelezwa kwa zaidi ya asilimia 90 ifikapo mwaka 2020.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuwahudumia wananchi na kuhakikisha huduma mbalimbali za kijamii kama maji, afya, nishati, elimu na miundombinu zinapatikana kwa uhakika.

Alitoa kauli hiyo jana jioni (Jumamosi, Februari 23, 2019) alipozungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika  katika uwanja wa Kituo cha Polisi  cha Tarakea wilayani Rombo, akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Kilimanjaro.

Waziri Mkuu alisema wananchi waendelee kuwa na Serikali yao ambayo imejipanga kutekeleza ahadi zote zilizotolewa na Rais Dkt. Magufuli kama Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya 2015-2020 inavyoelekeza.

Pia, Waziri Mkuu alisema mtumishi mzembe, mwizi, mla rushwa na asiyewajibika hana nafasi katika Serikali ya Awamu ya Tano, hivyo ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa watumishi wote waimarishe utendaji wao.

Waziri Mkuu alisema kila mtumishi wa umma anatakiwa ahakikishe anafanya kazi kwa bidii ili kuiwezesha Serikali kutimiza lengo lake la kuboresha maendeleo ya wananchi kwenye maeneo mbalimbali nchini hususani ya vijijini.

“Iwapo watumishi wa umma watatimiza majukumu yao ipasavyo changamoto nyingi zinazowakabili wananchi kama upatikanaji wa maji zitakuwa historia kwa kuwa Serikali inatoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.”

Waziri Mkuu alisema kwa sasa Serikali inatekeleza Kampeni ya Rais Dkt. Magufuli ya kumtua mama ndoo kichwani, ambapo itahakikisha kwamba wananchi wote wanapata huduma ya maji karibu na makazi yao.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu aliwaagiza viongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Rombo kwa kushirikiana na Madiwani wahakikishe wanaboresha masoko katika mipaka ya Holili na Tarakea ili yawe katika viwango vya kimataifa.

Waziri Mkuu alisema iwapo masoko hayo yaliyo katika mpaka wa Tanzania na Kenya yataboreshwa yatawavutia na wananchi wa Kenya kuja kufanyabiashara, hivyo kuiwezesha halmashauri hiyo kuongeza mapato.

Awali, Waziri Mkuu ambaye ameambatana na mkewe Mary alizungumza na watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Rombo katika ukumbi wa shule ya Sekondari ya Shauritanga na kisha waliweka mashada ya maua kwenye kaburi la pamoja la wanafunzi wa shule hiyo waliofariki dunia kwa ajali ya moto Juni 18, 1994.

Pia, Waziri Mkuu alitembelea kituo cha afya cha Karume kilichopo Usseri ambacho na kuzindua maboresho kituo hicho, ambacho kwa sasa kina uwezo wa kutoa huduma za upasuaji, mama na mtoto na maabara. Baada ya hapo alitembelea kituo cha forodha cha Tarakea.

Kwa upande wao, wananchi waliipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuwaboreshea huduma mbalimbali za jamii kama upatikanaji wa dawa na vipimo kwenye vituo vya kutolea huduma za afya, ambapo hapo awali hazikuwa na uhakika.

Mmoja wa wananchi hao, Maria Aristidi ambaye amelazwa katika kituo cha afya cha Karume baada ya kujifungua kwa njia ya upasuaji, aliishukuru Serikali kwa sababu awali hakukuwa na chumba cha upasuaji kwenye kituo hicho.

(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
chn
ap
Loading...
ad

Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
Mgid
taboola apo chini
hapa
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )