Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB,
Abdulmajid Nsekela amemshukuru Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan
kwa kukubali kuwa mgeni rasmi katika mbio za kwanza za hisani za “CRDB
Bank Marathon” zinazolenga kuhamasisha uchangiaji wa shilingi milioni
200 kusaidia gharama za matibabu kwa watoto 100 wenye uhitaji wa
upasuaji wa moyo. Nsekela ameeleza hayo katika mkutano na waandishi wa
habari uliofanyika katika makao makuu ya Benki ya CRDB, Azikiwe Jijini
Dar es Salaam.
Nsekela
alisema mbali na makamu wa Rais, viongozi mbalimbali ikiwamo Rais
mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete pamoja na Waziri wa Michezo,
Harisson Mwakyembe wanatarajiwa kuungana na maelfu ya wakimbiaji
kushiriki CRDB Bank Marathon tarehe 16 Agosti, 2020 katika viwanja vya
“The Greens” Oysterbay, Dar es Salaam.
“Kauli
mbiu ya mbiu yetu katika mbio hizi za hisani ni ‘Kasi Isambazayo
Tabasamu’, ikihamasisha watu wengi zaidi kujitokeza kushiriki kuleta
tumaini la maisha na kusambaza tabasamu kwa Watoto wenye magonjwa ya
moyo,” aliongezea Nsekela huku akibainisha kuwa CRDB Bank Marathon mwaka
huu inategemea kuwa na washiriki zaidi ya 4,000.

Mkurugenzi
Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (katikati) akizungumza
katika mkutano na Waandishi wa habari wakati wa kutambulisha mbio za
hisani “CRDB Bank Marathon 2020” zinazoandaliwa ili kuhamasisha
uchangiaji wa fedha kwa ajili ya upasuaji kwa watoto wenye magonjwa ya
moyo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete jijini Dar es salaam, leo.
Nsekela alisema CRDB Bank Marathon inatarajiwa kukusanya shilingi
milioni 200 ambapo washiriki zaidi ya 4,000 wanatarajiwa kushiriki siku
hiyo tarehe 16 Agosti,2020 jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi
Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete, Prof. Mohamed Janabi na
kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Sanlam Insurance, Khamisi Suleiman.
Akizungumzia
ushirikiano uliopo baina ya Benki ya CRDB na Taasisi ya Moyo katika
kusaidia matibabu kwa watoto wenye matatizo ya moyo, Nsekela alisema kwa
Benki ya CRDB imekuwa ikitoa msaada wa gharama za matibabu ambapo mwaka
jana ilitoa shilingi milioni 100 kwa ajili ya upasuaji wa moyo kwa
Watoto 50 na mapema mwaka huu ilitoa shilingi milioni 50 kwa ajili ya
Watoto 25.
“Pamoja
na jitihada za Serikali kupitia Taasisi ya Moyo kwa kushirikiana na
wadau wengine ikiwamo Benki yetu ya CRDB bado watoto wengi wamekuwa
wakikosa matibabu kutokana na wazazi au walezi kutomudu gharama za
upasuaji ambazo ni kati ya Shilingi Milioni 2 hadi Milioni 20,” alisema
Nsekela huku akibainisha kuwa CRDB Bank Marathon inatoa fursa kwa wadau
mbalimbali ikiwamo watu binafsi na Taasisi kushiriki kuchangia matibabu.
Nsekela
alizishukuru taasisi za Sanlam, Strategis, Alliance, ARIS, Cool Blue,
EFM na TVE na wengineo kwa kujitokeza kushirikiana na Benki ya CRDB
kufanikisha CRDB Bank Marathon, huku akihamasisha watu wengi zaidi
kujitokeza kushiriki kwa kujisali kupitia tovuti maalum ya
crdbtz.co/marathon.
“Kujisajili
ni rahisi sana, unaweza kujisajili binafsi na kuchangia shilingi 30,000
au kupitia vikundi na kuchangia 25,000 kwa kila mmoja kupitia matawi ya
Benki ya CRDB, CRDB Wakala, SimBanking App na mitandao ya simu (M-Pesa,
TigoPesa, AirtelMoney). Fedha hizi zote zitaelekezwa katika kusaidia
gharama za upasuaji wa watoto wenye magonjwa ya moyo,” alisema Nsekela.

Mkurugenzi
Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete, Prof. Mohamed Janabi
(kulia) akizungumza katika mkutano na Waandishi wa habari wakati wa
kutambulisha mbio za hisani “CRDB Bank Marathon 2020” zinazoandaliwa ili
kuhamasisha uchangiaji wa fedha kwa ajili ya upasuaji kwa watoto wenye
magonjwa ya moyo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete jijini Dar es
salaam, leo.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Profesa
Mohamed Janabi aliishukuru Benki ya CRDB kwa kuwa mstari wa mbele
kusaidia jitihada za utoaji huduma za upasuaji moyo kwa Watoto. Profesa
Janabi alitumia fursa hiyo pia kuwahamasisha Watanzania kujisajili kwa
wingi kushiriki mbio hizo za hisani ili kusaidia upasuaji kwa watoto.
“Takwimu
zinaonyesha watoto milioni 2 wanazaliwa nchini Tanzania wakati asilimia
1 kati yao huwa na magonjwa ya moyo. Ni wajibu wetu sisi kama jamii
kuhakikisha watoto hawa wanapata matibabu stahiki, hivyo ushiriki wetu
katika mbio hizi za hisani utusaidia kusambaza tabasamu kwa watoto hawa”
alisema Profesa Janabi.

Akihitimisha
mkutano huo Nsekela alisema Benki ya CRDB imejiwekea Sera maalum ya
kusaidia jamii “Corporate Social Responsibility Policy” ambayo
inaelekeza asilimia 1 ya faida ya kutumika katika kusaidia jamii katika
sekta za elimu, afya na mazingira, ambapo mwaka jana pekee Benki ilitoa
zaidi ya shilingi bilioni 1.2.
“Uanzishwaji
wa mbio za hisani za CRDB Bank Marathon utasaidia kuongeza ushiriki wa
wadau wengi zaidi katika Maendeleo katika sekta hizi za afya, elimu na
mazingira,” alisema Nsekela.
Loading...
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi
==>>... << BOFYA HAPA Kui Install>>
Mgid
hapa
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )